Sunday, November 13, 2011

Mchagua Jembe si Mkulima
Ng'ombe
Mchagua jembe si mkulima. Ndivyo wanavyosema waswahili. Ukiwa na nia ya kufanya kazi ama jambo lako, basi huwezi kutafuta sababu za kuikwepa kazi hiyo. Mara hoo sina hiki, wala kile, mkulima halisi atatafuta njia ya kupambana na mazingira yake.
Binti mmoja wa kijerumani, ameamua kutochagua jembe kwa kile anachotaka kufanya. Msichana huyu alitamani sana kupanda farasi, lakini, bahati mbaya nyumbani kwao, wazazi wake walikuwa hawamiliki farasi. Aliwaomba wazazi wake wampatie farasi, lakini wakamwambia kuwa hawana uwezo wa kumpata farasi, kwani wao ni wafuga ng’ombe.
Kama wasemavyo waswahili, penye nia pana njia. Msichana aliamua kumtumia ng’ombe huyo huyo aliyepatikana nyumbani. Alichukua vifaa vyote vinavyotumika kumpanda farasi ikiwa ni pamoja na matandiko na kuyaweka mgongoni kwa ng’ombe wao aitwaye RUNA.
Taratibu alianza kumfundisha ng’ombe kuruka viunzi kama farasi huku akiwa amempanda. Alimrusha kiunzi kimoja hadi kingine, na hatimaye baada ya miaka miwili, ng’ombe RUNA akafuzu.
Majirani za msichana huyu mwanzoni waliona kuwa alikuwa akifanya mchezo wa kitoto, lakini sasa wanamshangaa, alivyomudu kumfanya ng’ombe aruke kama farasi huku akitii amri zote anazopewa, hatimaye kupata tuzo ya Olimpiki. Faida za kutochagua jembe. Ruka ng’ombe, ruka!

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home